Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa jana amehamia rasmi mkoani Dodoma ili kutekeleza agizo la Serikali ya awamu ya tano kuhamia mkoani humo ambako ndiyo makao makuu ya nchi.
Amepokewa na viongozi mbalimbali wakiongozwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Walemavu, Jenister Mhagama na mamia ya wakazi wa Dodoma.
Ndege iliyombeba Waziri Mkuu iliwasili uwanja wa ndege saa 10.06 alasiri, ambapo alishuka ndani ya ndege akiwa ameongozana na mkewe, Mary, kisha kuwapungia wananchi.
Nje ya uwanja wa ndege, wananchi walijipanga barabarani wakiwa wamesimama na mabango, kama ishara ya kumkaribisha mkoani hapa kiongozi huyo wa juu, ambaye aliahidi Watanzania kuwa angehamia rasmi Dodoma mwezi Septemba.
Kutoka Uwanja wa Ndege wa Dodoma kwenda makazi ya Waziri Mkuu yaliyopo eneo la Mlimwa, wananchi wenye baiskeli, pikipiki na wengineo walijipanga kandokando ya barabara huku wakipunga matawi ya miti kuonesha furaha yao ya serikali kuanza kuhamia Dodoma.
Akizungumza nyumbani kwake, Majaliwa amesema waliosema serikali haiwezi kuhamia Dodoma wameumbuka, kwani serikali imehamia rasmi na wanaohitaji huduma ya Waziri Mkuu wataifuata Dodoma.
Amesema kitendo cha serikali kuhamia Dodoma, si tukio la kawaida. Alisema amefarijika kuona barabara nzima, zilijaa watu wenye furaha kwa ajili ya kumkaribisha Dodoma.
Pia amesema kuanzia leo serikali iko Dodoma; na yeyote anayeitaka huduma ya Waziri Mkuu, ataipata Dodoma. Alisema Dodoma ina uwezo wa kupokea watumishi wote wa serikali na wakaweza kufanya kazi zao kikamilifu.