Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema hospitali mpya ya kisasa itajengwa Binguni Wilaya ya Kati Unguja ikiwa na hadhi ya Hospitali ya Rufaa yenye uwezo wa kutoa huduma zote za matibabu kwa wananchi wa Unguja na Pemba.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Afya, Mahmoud Thabit Kombo wakati akijibu swali la Mwakilishi wa Jimbo la Tunguu, Simai Mohamed Said aliyetaka kujua ni lini ujenzi wa hospitali hiyo utaanza.
Kombo amesema hatua za ujenzi wa hospitali ya kisasa Binguni ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na ahadi ambazo zilitolewa na mgombea urais wa Zanzibar kwa tiketi ya chama hicho katika kampeni za uchaguzi mkuu, mwaka jana.
Amesema utekelezaji wa ahadi hiyo upo na utatekelezwa kwa vitendo kwa lengo la kuimarisha huduma za afya kuweza kuwafikia wananchi wote kwa ubora unaostahili. Akitoa mfano alisema katika hospitali mpya ya Binguni Wilaya ya Kati Unguja huduma zote za vitengo vya afya zitapatikana ikiwemo ya matibabu ya saratani.
Amesema uamuzi wa ujenzi wa Hospitali ya Binguni umekuja baada ya hospitali iliyopo sasa ya Mnazi Mmoja kuzidiwa na idadi kubwa ya watu, ikiwemo wagonjwa wanaotoka sehemu zote mbili za Unguja na Pemba.