Mahakama moja nchini Kenya imemhukumu mshukiwa wa ugaidi kifungo cha miaka 80 jela.
Abdi Rizzack muktar Edow kwanza alihukumiwa kifungo cha miaka 20 jela alipopatikana na hatia ya kufadhili na kufanikisha ugaidi nchini Kenya.
Mfanyibiashara huyo mwenye umri wa miaka 24 alihukumiwa kifungo kingine cha miaka 10 kwa kila kosa, kwa makosa mengine sita ikiwemo kuwashawishi na kuwasajili vijana kujiunga na kundi la kigaidi Al shabab.
Hakimu mkuu bi Joyce Gandani alisema ni dhahiri kuwa Muktar Edow alikuwa na nia ya kuvuruga amani nchini Kenya kwa hivyo mbinu zote sharti zitumike kulinda maisha ya wakenya na maafisa wa usalama kutoka kwa watu wenye nia kama yake.
Edow alikamatwa katika mbuga ya wanyama pori ya Maasai Mara Juni mwaka 2014 siku moja baada ya gari lake kunaswa na maafisa wa usalama likiwa limewabeba wapiganaji wa kundi la Al shabab walipoendesha uvamizi katika mji ulioko Kaskazini mwa Kenya Mandera.