Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba amesema kuwa bado anatambua yeye ni mwenyekiti halali wa chama hicho.

Lipumba amesema atampokea Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad siku atakapofika kwenye ofisi hiyo makao makuu Buguruni kwa ajili ya kuandaa mikakati ya kukijenga chama hicho.

Profesa Lipumba amesema kikao cha Baraza Kuu la Uongozi Taifa kilichofanyika Zanzibar ni batili kwa kuwa walikiuka katiba ya chama hicho.

Pia amsema, kwa mujibu wa kifungu cha 79(2)(a) cha katiba ya chama hicho kinasema kuwa, Mkutano Mkuu wa Taifa unaweza kuchukua hatua za kinidhamu zozote zile, zikiwamo kumuachisha au kumkufukuza uongozi au uanachama au yote mawili Mwenyekiti wa chama hicho.

Alisema pamoja na kufanyika kwa kikao hicho, lakini pia idadi ya wajumbe waliohudhuria kutoka Bara ni 9 ambao kati yao, watatu wajumbe wa kamati kuu na sita ni wanachama wa kawaida, wakati Katiba ya chama hicho kinawataka kuwa na wajumbe 22 kutoka Kamati Kuu ya chama.

Profesa Lipumba alisema, katika katiba hiyo, pia kifungu cha 83(5) kinasema, baraza hilo linaweza kuchukua hatua za kinidhamu ikiwa ni pamoja na kutoa onyo kwa maandishi, karipio kali.

Amesema kabla ya kufikia uamuzi huo, Katibu Mkuu alipaswa kuitisha Mkutano Mkuu ambao pamoja na mambo mengine, ulitakiwa kumjadili ili wajumbe waweze kumpigia kura ya kumwondoa. Pia alisema alipaswa kupewa nafasi ya kujieleza katika mkutano mkuu ndipo wajumbe waamue hatua ya kumchukulia.

Kutokana na hayo alisema yeye bado ni mwenyekiti halali na yupo ngangari katika kukijenga chama na hafukuziki, hasusi wala hawezi kukihama chama hicho badala yake amejiwekee mikakati ya kuhakikisha anawaunganisha wanachama wa chama hicho.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *