Rais wa Jamhuri ya Mungano wa Tanzania, John Magufuli amezindua ndege mbili za Serikali kwenye hafla iliyofanyika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Julius Kambarage Nyerere jijini Dar es Saalam.

Hafla hiyo imehudhuriwa pia na Waziri wa Ujenzi Mawasiliano na Uchukuzi Profesa Makame Mbawara, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Saalam Paul Makonda, Mstahiki Meya wa Jiji la Dar es Saalam Isaya Mwita na viongozi wengine mbalimbali.

Vilevile rais aliwawaumbua watu wote wanaobeza ununuzi wa ndege hizo na kuziita zina kasi ndogo ya Bajaj akawataka wawe na moyo wa kupenda vitu vyao wenyewe.

Pia amewahakikishia Watanzania kwa ujumla kwamba ndege hizo ni mpya na zimenunuliwa kwa pesa taslimu na kwamba malipo yake yalifanyika kwa awamu mbili.  Awamu ya kwanza serikali ililipa asilimia 40 na baada ya kukamilika utengenezaji wake ilimalizia asilimia 60 iliyobaki.

Rais  pia ametoa onyo kwa bodi mpya ya ATCL kuhusu dhamana waliyokabidhiwa na kuwaambia wanatakiwa kulisimamia shirika hilo kwa weledi ili liweze kujitegemea.

Ndege hizo zitakuwa mali ya serikali na zitakodishwa kwa ATCL kwa mkataba maalum ambapo amesema lazima uwepo mkataba wa makabidhiano.

Mkataba huo utakuwa kati ya katibu mkuu kiongozi, katibu mkuu wizara ya uchukuzi na mawasiliano na mtendaji mkuu wa ATCL ambao ndiyo wamepewa dhamana ya kuzisimamia ndege hizo.

Ndege hizo zenye sifa ya matumizi madogo ya mafuta zitakuwa suluhisho la kupanda kwa bei ya usafiri wa anga nchini na pia zitasaidia kukuza sekta ya utalii nchini.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *