Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli amepokea msaada wa Shilingi Milioni 545 kutoka kwa Waziri Mkuu wa India Mhe. Narendra Modi kwa ajili ya kusaidia wananchi wa Mkoa wa Kagera waliopatwa na maafa ya tetemeko la ardhi lililotokea tarehe 10 Septemba, 2016.
Hundi ya fedha hizo imekabidhiwa Ikulu Jijini Dar es Salaam na Balozi wa India hapa nchini Mhe. Sandeep Arya na baadaye Rais Magufuli akaikabidhi kwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa.
Katika barua yake kwa Rais Magufuli iliyosomwa na Balozi Sandeep Arya, Waziri Mkuu wa India Mhe. Narendra Modi amesema Serikali na Wananchi wa India wamepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za kutokea kwa maafa hayo yaliyosababisha vifo vya watu na uharibifu wa mali.
Kwa Upande wake Rais Magufuli amemshukuru Waziri Mkuu wa India Mhe. Narendra Modi na Serikali yake kwa kutoa mchango huo na kutuma salamu za rambirambi, na amesema Serikali yake imeguswa na moyo wa upendo waliounesha.