Makampuni ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL) na Pan Africa Power Solutions (PAP) Tanzania Limited, yameungana na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kupinga uamuzi uliotolewa hivi karibuni na Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Migogoro ya Kibiashara (ICSID) kuilipa Benki ya Standard Chartered ya Hong Kong (SCBHK) kiasi cha dola za Marekani milioni 148.4.

Msimamo huo pia umetolewa na aliyekuwa mwanahisa wa kampuni ya IPTL, VIP Engineering and Marketing Limited, ambayo imedai kuwa deni ambalo SCBHK inashinikiza ilipwe na Tanesco, limegubikwa na utata mwingi wa kisheria.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mwanasheria wa IPTL na PAP, Joseph Makandege, alisema ameshitushwa na amri iliyotolewa na ICSID kwa manufaa ya SCBHK, ambayo ilifungua shauri hilo kama wakala wao.

Makandege alibainisha kuwa kutokana na vitendo vya SCBHK, kuendelea kujitangaza kuwa mdai wa IPTL, PAP ilifungua shauri la madai namba 60/2014 Mahakama Kuu. Katika shauri hilo, PAP inadai nafuu kadhaa ikiwepo Mahakama Kuu kutamka kuwa benki hiyo sio mdai wa IPTL na kwamba ilipe fidia ya dola za Marekani bilioni 3.24, ambazo ni takribani trilioni 6.48 za Tanzania.

Makandege alidai pia kuwa amri ya ICSID, imekiuka maamuzi yaliyotolewa na Mahakama Kuu mbele ya Jaji Fauz Twaib, ambaye alitoa zuio kwa Tanesco na hao Benki ya Standard Chartered ya Hong Kong, kutokukaa na kukokotoa bei ya umeme mpaka shauri liliofunguliwa na PAP litakapotolewa uamuzi.

Kwa upande wake, wakili wa VIP, Dk Camilo Schutte, alieleza katika mahojiano maalumu kuwa msimamo wa wateja wake ni kuona kuwa maamuzi ya ICSID hayatekelezwi, kwa vile kuna mapungufu makubwa yaliyosababisha maamuzi hayo na kuwaomba Tanesco kuchukua hatua bila kuchelewa.

Amefafanua kuwa deni la dola za Marekani milioni 120 SCBHK inayoshinikiza lilipwe, halikuidhinishwa na IPTL, bali na Mechmar Corporation (Malaysia) Berhad (Mechmar), kwa vile VIP, ambaye ni mbia mwenza na bodi yake, haikushirikishwa na mpango huo ulikuwa unajulikana hata kwa Benki yenyewe.

Kauli ya Tanesco Alhamisi wiki iliyopita, Mkurugenzi Mkuu wa Tanesco, Felchesmi Mramba alisema Bodi ya Wakurugenzi ya shirika hilo, imepanga kukata rufaa dhidi ya uamuzi uliotolewa na Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Kibiashara (ICSID) ya Uingereza ya kulitaka shirika hilo kuilipa Benki ya Standard Chartered ya Hong Kong (SCB-HK) Dola za Marekani milioni 148.4 (sawa na Sh bilioni 320).

Fedha hizo ni malimbikizo ya gharama za uwekezaji wa mitambo ya kuzalisha umeme ya Kampuni ya Independent Power Tanzania (IPTL), Tegeta jijini Dar es Salaam. Mramba alisema mpango huo wa kukata rufaa, unatokana na kukiukwa kwa sheria na kanuni kadhaa zinazosimamia uendeshaji wa Mahakama hiyo tangu ilipofunguliwa mwaka 2010, ilipotoa uamuzi wa awali mwaka 2014 hadi ilipotoa uamuzi wa mwisho hivi karibuni.

Alisema katika uamuzi wa hivi karibuni, Mahakama hiyo ilishindwa kuzingatia uamuzi wake wa awali wa mwaka 2014, na kutoa maamuzi mapya, kama vile kesi hiyo imeendeshwa upya, jambo ambalo ni kinyume na matakwa ya sheria na kanuni za uendeshaji wa Mahakama hiyo.

Alisema kutokana na uamuzi huo, Tanesco itawatumia wakili wake, Richard Rweyongeza wa Kampuni ya R.K Rweyongeza & Advocates, kukata rufaa hiyo ndani ya siku 90 zilizotolewa na Makakama ya ICSID.

Pamoja na uamuzi wa juzi kutokuwa mpya ukilinganisha na ule wa awali uliotolewa na Mahakama hiyo ya Kimataifa Februari 12, 2014, huku ukitoa nafuu zaidi kwa Tanesco, lakini shirika hilo limesisitiza kuwa bado yapo maeneo ambayo kama yataangaliwa kwa kina katika rufaa yao, yatatoa nafuu zaidi wa uamuzi wa mwisho wa fedha inayopaswa kulipwa, lakini pia mhusika halali wa kulipwa tofauti na ilivyoamriwa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *