Yanga SC jana imepokea kichapo cha 1-0 kutoka kwa Stand United kwenye mechi ya ligi kuu Tanzania Bara iliyofanyika katika Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga.

Yanga ni bingwa mtetezi wa ligi hiyo na hicho ni kipigo chake cha kwanza katika ligi hiyo inayoshirikisha timu 16, pia alikuwa mwakilishi wa mwisho wa Tanzania katika mashindano ya kimataifa baada ya timu zingine kutolewa mapema.

Katika mchezo wa jana, Pastor Athanas ndiye aliyewalaza mapema mashabiki wa Yanga baada ya kufunga bao hilo pekee katika kipindi cha kwanza cha mchezo huo uliohudhuriwa na watazamaji wengi.

Mchezaji huyo alifunga bao hilo baada ya pasi safi kutoka kwa mchezaji mwenzake Kelvin Sabato aliyemtoka beki wa Yanga, Vicent Bossou.

Baada ya kumtoka beki huyo alikimbia kwa kasi na kisha kumpangua kipa wa Yanga Ally Mustapha `Barthez’ na kisha kuachia shuti kali lililomwacha kipa huyo akiwa chini. Stand United ilicheza mchezo huo huku ikiwa inashangiliwa mwanzo mwisho wa mchezo na mashabiki wao ambao walikuwa wameujaza uwanja huo.

Kwa ushindi huo, Stand United imefikisha pointi 12 na kupanda kutoka nafasi ya nne hadi ya pili nyuma ya Simba inayoshikilia uongozi ikiwa na pointi 16, huku Yanga ikishuka hadi nafasi ya tatu kutoka ya pili na kubaki na pointi zake 10.

Yanga yenyewe inaendelea kubakia nafasi ya tatu ikiwa na pointi 10 sawa na Mtibwa Sugar, lakini zikitofautiana kwa uwiano wa mabao.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *