Shirika lisilo la  Kiserikali    la Speak  Up for Africa    limemtunuku tuzo, rais mstaafu, Jakaya Kikwete, kutokana na uongozi wake wa kisiasa na utetezi wake  kwa  makundi ya jamii yaliyo katika mazingira magumu hususani wanawake na watoto.

Utoaji wa  tuzo hiyo  ya  uongozi wa kisiasa na utetezi , umekwenda sambamba na   hafla ya  miaka mitano ya kuanzishwa kwa  Taasisi ya Speak up  Africa.

Hafla  hiyo iliyofanyika jana Alhamisi Jijini New York   ilikuwa  pia  ni sehemu ya kuhamasisha uchangiaji   wa shughuli za  taasisi hiyo.

Mchango ambao umetambuliwa na  Speak Up  Africa,   taasisi ambayo imekuwa ikifanya kazi  kwa karibu na Kikwete, ni  katika maeneo ya  upelekaji na usambazaji wa huduma za msingi za afya hususani afya ya mama na mtoto,  udhibiti wa  ugonjwa  wa malaria kupitia kampeni  ya Malaria Haikubaliki, usambazaji wa vyandarua  vyenye viatilifu, kampeni ya  lishe bora, na  kampeni ya   chanjo kwa watoto.

Pamoja  na  kutambua  juhudi zake katika  kuyasemea maeneo hayo,  taasisi hiyo kupitia  Mkurugenzi wake  Mtendaji Bi. Kate Campana pia imemtambua  kama kiongozi ambaye    amekuwa mstari wa mbele  wa kulisemea Bara la Afrika kila  mara alipopata  fursa  ya  kufanya hivyo wakati akiwa madarakani na hata baada ya kustaafu.

Kikwete ameelezwa katika hafla hiyo iliyowashirikisha  wadau wa kada mbalimbali, kama kiongozi wa kisiasa ambaye amezigusa nyoyo za watu wengi kujitolea kwa ajili ya watu wenye mahitaji ya kupata huduma za msingi za kijamii ambazo  au wameshindwa kuzipata kutokana na kipato kidogo au haziwafikii kabisa.

Akipokea  tuzo hiyo, amesema tuzo hiyo ni ya watoto wote  Waafrika ambao ndiyo  waliomfanya asimame   mbele ya wageni waalikwa.

Amesema anamini katika ushirikiano na wadau mbalimbali  kama akina Ray Chambers kupitia kampeni ya  Hakuna Tena Malaria, Taasisi ya  Billy na Melinda Gates na Gavi Vaccination   Alliance ambayo anashirikiana  nayo kwa karibu katika  kampeni ya chanjo kwa wote.

Kikwete amewahakikishia   watendaji wa Speak  Up Africa kwamba  ataendelea kufanya kazi nao kwa karibu  kutokana  kile alichosema amejionea mwenye kazi nzuri wanayoifanya.

Wengine waliopewa tuzo kwa kutambua michango yao kwa jamii ni  pamoja na   Professa Awa Marie Coll- Seck, Waziri wa Afya  wa Senegal, Bibi Toyin  Saraki,  mwanzilishi wa Taasisi ya  Wellbeing  Afrika ambayo  pia imekuwa ikitoa  elimu na misaada kwa wanawake na watoto pamoja na elimu  kwa wakunga na kutambua kazi nzuri, kubwa na ngumu  ya kuwahudumia wanawake wenzao wanapojifungua. Pia alikuwemo Kabirou Mbodje ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa  Taasisi ya  Wari.

Taasisi ya  Speak  Up  Africa  imeanzishwa  na wanawake na inaongozwa na wanawake. Ni taasisi ambayo imejijengea uwezo na sifa kubwa ndani  ya kipindi cha miaka mitano tangu  kuanzishwa kwake.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *