Mahakama ya Rufaa leo inatarajia kutoa uamuzi wa rufaa ya aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Dar es Salaam (RCO) Kamishna Msaidizi wa Polisi Abdallah Zombe na maofisa wenzake watatu.
Hukumu hiyo itahitimisha mvutano wa muda mrefu wa kisheria kati ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) na maofisa hao.
Wajibu rufani wengine ni Mrakibu wa Polisi (SP) Christopher Bageni, aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi Wilaya ya Kinondoni (OC-CID); aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi wa Kituo cha Polisi Urafiki, Mrakibu Msaidizi wa Polisi (ASP) Ahmed Makelle na Rajabu Bakari.
Habari kutoka mahakamani hapo zilizothibitishwa na Msajili wa Mahakamahiyo, John Kahyoza hukumu inatarajiwa kusomwa leo saa sita mchana.
Hukumu hiyo ambayo imekuwa ikisubiriwa na wadau, wakiwamo ndugu wa marehemu hao, wanasheria na jamii kwa jumla inatolewa leo baada ya miezi minne, majuma mawili na siku mbili, tangu rufaa iliposikilizwa.
DPP alikata rufaa akipinga hukumu ya Mahakama Kuu iliyowaachia huru Zombe na wenzake wanane katika kesi ya mauaji ya wafanyabiashara wawili wa madini kutoka Mahenge, Morogoro na dereva wa teksi, mkazi wa Dar es Salaam.
Katika kesi ya msingi, Zombe na wenzake walidaiwa kuwaua kwa kukusudia wafanyabiashara Sabinus Chigumbi, maarufu Jongo na ndugu yake, Ephrahim Chigumbi, Mathias Lunkombe na Juma Ndugu, aliyekuwa dereva wa teksi wa Manzese.
Walidaiwa kutenda makosa hayo Januari 14, mwaka 2006, katika msitu wa Pande, uliopo wilayani Kinondoni baada ya kuwakamata wafanyabiashara hao Sinza, walipokuja Dar es Salaam kuuza madini.
Agosti 17, 2009, Mahakama Kuu iliwaachia huru washtakiwa hao ikisema baada ya kusikiliza ushahidi na hoja za mawakili wa pande zote iliridhika kuwa hawakuwa na hatia ya mashtaka yaliyokuwa yakiwakabili.
Badala ya kosa la mauaji ambalo adhabu yake ni kunyongwa hadi kufaa, DPP aliiomba Mahakama imtie hatiani Zombe kwa kosa la kuwalinda wahalifu (wanaodaiwa kutenda kosa la mauaji hayo), ambalo adhabu yake ni kifungo kisichozidi miaka saba jela.
Wakili wa Serikali Mkuu (PSA), Timon Vitalis alidai DPP alifikia uamuzi huo baada ya kujiridhisha kuwa hakuna ushahidi wa kumtia hatiani Zombe kwa kosa la mauaji.
Kabla ya kubadili msimamo huo dhidi ya Zombe, DPP aliwafutia rufaa wajibu rufani watano, Jane Andrew, Emmanuel Mabula, Michael Shonza, Abineth Salo na Festus Gwabisabi.