Mwenyekiti wa Umoja wa Maofisa Watendaji Wakuu wa Kampuni Binafsi nchini Tanzania (CEO round table), Balozi Ali Mufuruki, amesema uchumi wa Tanzania haujatetereka kama ambavyo imekuwa ikielezwa na baadhi ya watu.
Mufuruki amesema kuwa uchumi safari hii ndiyo umezidi kuimarika zaidi kutokana na hatua kadhaa za kiuchumi zinazochukuliwa na serikali ya awamu ya tano.
Balozi Mufuruki amesema wanaotoa hoja hizo hawana ushahidi wa kisayansi kwani takwimu zinaonesha kuwa tangu serikali ya awamu ya tano iingie madarakani, mfumuko wa bei umekuwa ukishuka siku hadi siku huku thamani ya shilingi nayo ikiendelea kuimarika.
Balozi Mufuki pia amezungumzia uamuzi wa serikali kuhamishia makao yake makuu mjini Dodoma na kuitaja hatua hiyo kuwa ni fursa nyingine ya kiuchumi kwa makampuni na wafanyabiashara binafsi kwenda kuwekeza wakati huo huo jiji la Dar es Salaam likipangwa upya na kuwa kitovu cha uchumi na utalii kama ilivyo miji ya Dubai, Hong Kong, Paris na New York.