Mgombea urais wa chama cha Democratic nchini Marekani Hillary Clinton amefuta mkutano wake wa kampeni jimbo la California baada yake kuugua.
Bi Clinton amechukua hatua hiyo baada ya kugunduliwa kwamba anaugua ugonjwa wa kichomi ambao pia hujulikana kama nimonia.
Kichomi ni ugonjwa wa mapafu. Dalili zake huwa ni pamoja na kukohoa, homa, uchovu, baridi na kutatizika wakati wa kupumua.
Jumapili, alilazimika kuondoka mapema kutoka kwenye hafla ya kukumbuka waathiriwa wa shambulio la kigaidi la 9/11 jijini New York.
Hafla hiyo ilikuwa ya kuadhimisha miaka 15 tangu kutekelezwa kwa shambulio hilo lililosababisha vifo vya karibu watu 2,900.
Saa chache baadaye, madaktari wake walisema alikuwa amegunduliwa kuwa anaugua ugonjwa wa kichomi siku mbili awali na kwamba alipewa dawa na kushauriwa kupumzika.
Baada ya kuondoka kwenye hafla hiyo ya Jumapili, ambapo video zilionesha akisaidiwa kutembea, alipelekwa nyumbani kwa dadake hapo karibu.
Bi Clinton alikuwa amepangiwa kuelekea California Jumatatu kwa ziara ya siku mbili, ambapo miongoni mwa mengine angehudhuria mikutano cha kuchangisha pesa na pia kutoa hotuba kuhusu uchumi.