Maafisa wa uchukuzi wa ndege nchini Marekani wamewatahadharisha abiria wanaosafiri kwa ndege kutofungulia au kuchaji simu za Samsung Galaxy Note 7 wakiwa ndani ya ndege.
Taasisi ya Uchukuzi wa Ndege Marekani (FAA) pia imewashauri watu kutoweka simu hizo kwenye mizigo ambayo wanaingia nayo eneo wanamoketi abiria kwenye ndege.
Kampuni ya Samsung ilisitisha uuzaji wa simu hizo na kukubali kwamba kulikuwa na hitilafu wakati wa uundaji wa betri za simu hizo.
Simu hizo zilidaiwa kulipuka zikiwekwa chaji au baada ya kuwekwa chaji.
Mashirika ya Australia ya Qantas na Virgin Australia pia yamewashauri wateja kutoweka chaji simu zao au hata kuzitumia wanaposafiri kwa ndege.
Kando na kasoro hizo, simu hiyo ambayo ilizinduliwa mwezi uliopita imefurahiwa na wateja na wakosoaji.
Simu takriban 2.5 milioni za Note 7 zilikuwa zimesafirishwa maeneo mbalimbali duniani.
Samsung wamesema wateja ambao tayari walikuwa wamenunua simu hizo na zimepata hitilafu watapewa fursa ya kuzibadilisha. Shughuli ya kupata simu mpya itachukua takriban wiki mbili.