Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya imewasimamisha kazi maafisa wake watatu, mmoja wamempa onyo kali na mwingine kushushwa cheo kutokana na watumishi hao kukumbwa na tuhuma mbali mbali ikiwemo ubadhilifu.

Maamuzi hayo yamefikiwa baada ya madiwani wa baraza la madiwani wa halmashauri kujigeuza na kuwa kamati katika kikao kilichoanza saa tatu asubuhi hadi sa tatu usiku.

Akitoa taarifa kwa Waandishi wa habari leo ofisini kwake, mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Amelchiory Biyego Kulwizila aliwataja Watumishi waliokumbwa na mkasa huo kuwa ni pamoja na muweka hazina Hafidhi Mgagi, anayekabiliwa na makosa mawili ambapo kosa la kwanza ni madeni ya walimu hewa ya shilingi milioni 115,630,000 ambazo hazikulipwa na zimetumika kwenye matumizi yasiyo julikana.

Kulwizila amesema mtumishi huyo pia anakabiliwa na kosa la pili ambalo ni upotevu wa pesa za Mradi wa Maji wa Horongo, Itimu na Mwampalala milioni 164.5 ambazo zililipwa bila vielelezo vinavyo onesha kama mkandarasi aliomba kufanya kazi hiyo.

Amemtaja Mtumishi wa pili kuwa ni Betty Mlaki Afisa Elimu Msingi ambaye anatuhumiwa kwa kosa la kutoa takwimu za uongo za idadi ya madawati na upotevu wa hela za umitashumta ambazo hazijatajwa kiwango.

Amesema Mtumishi wa Tatu ni Elissa Msana, ambaye ni Afisa Ugavi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya ambaye anatuhumiwa kwa kosa la kupitisha mikataba mibovu.

Mkurugenzi huyo amesema mtumishi wa nne ni Edwini Magili ambaye ni mhandisi wa halmashauri ambapo anatuhumiwa kwa kosa la kusimamia vibaya mradi wa madawati na kwamba baraza limeampa adhabu ya onyo kali.

Ameongeza kuwa mtumishi wa tano ni Roveli Ng’ambi ambaye alikuwa ni kaimu mhandisi wa maji ameondolewa nafasi yake ya kukaimu kutokana na usimamizi mbovu wa Mradi wa Maji Horongo, Itimu na Mwampalala.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *