Spika wa Bunge, Job Ndugai amewarejesha ndani ya ukumbi wabunge wa Upinzani lakini akawaambia kuwa wanatakiwa kuwa na umoja, ustahimilivu, busara, hekima, kuzingatia Kanuni na Sheria pamoja na lugha zenye staha.

Alitumia fursa hiyo kuwaasa wabunge kutimiza majukumu yao kwa kuzingatia busara, hekima, ustahimilivu na umoja huku wakitakiwa kujenga hoja ushawishi na matumizi ya lugha zenye staha wakati wa vikao vya Bunge ili kujiepusha na mihemko ndani ya Bunge.

Alimshukuru Mungu kwa uponyaji na kumuwezesha kurudi tena nyumbani na bungeni kuongoza Mkutano wa Nne wa Bunge la 11 ulioanza jana mjini hapa, uliohudhuriwa na wabunge wa Kambi ya Upinzani waliokuwa wamesusa vikao vya Bunge la Bajeti Juni mwaka huu.

Ndugai pia alimshukuru Rais John Magufuli kwa kufuatilia matibabu yake na afya yake kwa ujumla, wabunge, viongozi wa dini, na wananchi kwa kumuombea wakati wote alipokuwa akipitia mapito ya kuugua.

Wakati Spika akishukuru na kurudi salama bungeni, wabunge wa upinzani (wa vyama vinavyounda Ukawa) wakiongozwa na Kiongozi wa Kambi ya Upinzani, Freeman Mbowe wamerejea bungeni na kuungana na wabunge wenzao kuendelea na shughuli za Bunge.

Akiendelea kutoa taarifa ya Spika, Ndugai alimshukuru pia daktari kiongozi aliyemtaja kwa jina moja la Dk Vijay kwa kuongoza matibabu yake aliyeshirikiana na mkewe, Dk Fatma na kuongeza kuwa ni ukweli usiopingika wanawake wanaweza.

Aliwashukuru viongozi wanaosimamia shughuli za Bunge kwa kuongoza vizuri Bunge la Bajeti la siku 70 lililoanza Aprili 9 hadi Juni 30, mwaka huu. Alimpongeza Naibu Spika Dk Tulia Ackson kwa kazi nzuri wakati hayupo na kwamba ni ya kupigiwa mfano.

Spika aliwapongeza wenyeviti wa Bunge, Mussa Azzan Zungu, Andrew Chenge na Najma Murtaza Giga na kuwataka waendelee kumpa ushirikiano kama walivyoshirikiana wakati hayupo.

Tofauti na matarajio ya wengi, hali ya amani na utulivu ilitawala bungeni licha ya ujio wa wabunge wa upinzani ambao walisusa Bunge kwa takribani mwezi mmoja hadi Juni 30, mwaka huu wakati wa Bunge la Bajeti lilipomaliza vikao vyake.

Mbali ya Mbowe, wengine waliokuwepo ni pamoja na Godbless Lema, Mchungaji Peter Msigwa, David Silinde, John Heche na wengineo. Katika hatua nyingine, Spika Ndugai alisema katika Mkutano wa Tatu miswada mitano ilipitishwa na kwamba Rais John Magufuli ameshaisaini na kupitishwa kuwa sheria.

Alizitaja sheria hizo kuwa ni Sheria ya Fedha na Matumizi ya Mwaka 2016, Sheria ya Fedha Namba 2 ya Mwaka 2016, Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali Namba 3 ya 2016, Sheria ya Marekebisho ya Pili Namba 4 ya 2016 na Sheria ya Marekebisho ya Ununuzi wa Umma Namba Tano, 2016.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *