Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amewahakikishia wananchi wa Zanzibar kuwa atasimamia kwa nguvu zote masuala yote yanayohusu maendeleo, kudumisha Muungano wa Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar na kudumisha amani kwa faida ya wananchi.

Rais Magufuli amesema hayo alipokuwa akizungumza na wananchi wa Zanzibar katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa Kibandamaiti Mjini Unguja.

Rais Magufuli amesema ili mambo hayo yafanikiwe Wananchi wa Zanzibar hawana budi kukataa kujihusisha na vitendo vya vurugu na kuvunja amani na amewaonya watu wanaochochea vitendo hivyo kuacha mara moja.

Rais huyo amewataka wananchi wa Zanzibar kujihadhari dhidi ya wanasiasa ambao wanapandikiza chuki, ubaguzi na fitina, kwani watu hao wanataka kubomoa misingi mizuri ya umoja, upendo na mshikamano wa Taifa uliojengwa na waasisi wa Taifa hili.

Vile vile Rais Magufuli amempongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Mohamed Shein kwa hatua mbalimbali anazozichukua kuwaletea maendeleo wananchi wa Zanzibar.

Pia Rais Magufuli amevipongeza vyombo vya ulinzi na usalama kwa kazi nzuri vinayofanya katika kusimamia amani visiwani humo huku akivihakikishia kuwa yeye akiwa kiongozi wao anawaunga mkono.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *