Chama Cha Waigizaji kutoka Kinondoni kimetoa pongezi kwa Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dk. John Pombe Magufuli kwa kazi yao nzuri tangu ishike madaraka.
Katibu wa chama hicho, Jafari Dionizi amesema anampongeza rais kwa kuunda Wizara ya Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo na kumteua Nape Nnauye ambaye ana kasi kubwa ya kugundua wizi mkubwa wa kazi za wasanii na kuwakamata wahalifu hao.
Pia katibu huyo ameongeza kwa kusema kwamba anamuomba Waziri Nape afanye zoezi hilo kuwa endelevu kwani litafanya wasanii kunufaika na matunda ya kazi zao.
Waigizaji hao wametoa pongezi hizo kufuatia ziara ya Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Nape Nnauye aliyeifanya katika mitaa ya Kariakoo na kubaini viwanda bubu vya uharamia wa kazi za filamu hapa nchini.
Baadhdi ya viongozi wa Chama hicho waliotoa pongezi hizo ni mwenyekiti wa chama hicho Ali Baucha pamoja na mjumbe wa chama Ahmed Olotu maarufu kama Mzee Chilo.
Waigizaji wanakabiliwa na changamoto ya kuibiwa kwa kazi zao kutokana na kutokuwa na ufuatiliaji wa karibu hapo awali ambapo maharamia hao wamekuwa wakihujumu kazi za sanaa kutoka kwa wasanii tofauti hapa nchini.