Waziri mkuu wa Japan, Shinzo Abe ameahidi kutoa dola bilioni 30 za kufadhili miradi ya maendeleo barani Afrika kwa lengo la kuimarisha ukuaji na biashara barani Afrika.
Theluthi ya pesa hizo za msaada zitatumika kufadhili miradi ya miundo mbinu barani Afrika.
Waziri mkuu huyo ametoa ahadi hiyo wakati wa ufunguzi wa kongamano la maendeleo barani Afrika linalofanyika nchini Kenya.
Kwa mara ya kwanza kongamano la sita la kimataifa la Tokyo kuhusu maendeleo barani Afrika (TICAD-VI) limeandaliwa barani Afrika.
Kongamano hilo limehudhuriwa na wajumbe 10,000 na marais zaidi ya thelathini kutoka nchi za afrika ambapo Japan inajaribu kurejesha ushawishi wake wa awali na masoko ya nje ambayo yamenyakuliwa na nchi ya China.