Mwanamuziki wa Bongo Fleva aliyewahi kutamba na ngoma yake ya Nilonge Nisilonge miaka kadhaa iliyopita, Hamis Juma Mbizo (H Mbizo) amefariki dunia.
Msiba wa H- Mbizo umetokea katika hospital ya mkoa wa Morogoro alipolazwa kwa wiki mbili kufuatia matatizo ya mgongo.
Mdau mkubwa wa sanaa, Juma Mbizo ambaye ni baba mzazi wa H- Mbixo, amesema kuwa mipango ya kuuleta mwili wa marehemu jijini Dar es Salaam imeanza kufanywa na mazishi yanatarajiwa kufanyika Jumapili saa saba mchana, makaburi ya Magomeni Ndungumbi.
Mbali na uimbaji, H- Mbizo pia alikuwa mmoja watunzi wazuri wa nyimbo za bongo fleva ambapo moja ya kazi yake iliyofanya vizuri sana ni “Majanga” ya Snura.
Kwa mujibu wa Juma Mbizo ambaye aliingia Morogoro usiku huu, mwanae alifariki dakika chache baada ya yeye kufika hospitalini kumjulia hali.
“Mungu ana makusudio yake, ni kama vile Hamis alikuwa ananisubiria mimi, amefariki muda mfupi baada ya kumwona,” alisema Juma Mbizo.
Tangu amerejea nchini kutoka Afrika Kusini, H Mbizo alikuwa akisumbuliwa na mgongo na hivi karibuni akaenda Morogoro kwa dada yake kwaajili ya mapumziko lakini baadae alizidiwa na kulazwa Hospitali ya Mkoa.
Msiba wa H Mbizo utakuwa nyumbani kwao Magomeni Makanya (Day Brake).
Katika uhai wake, H – Mbizo pia aliwahi kuzitumikia kwa kipindi kifupi bendi za dansi za Chuchu Sound na Twanga Pepeta.