Mtayarishaji mkongwe wa muziki Bongo Fleva, P Funk Majani amesema wasanii wengi wa muziki wa Bongo Fleva wanapenda kulalamika kuhusu haki zao lakini wakipewa fursa ya kutoa maoni yao ili sheria ama kanuni zitungwe kuboresha wanakwepa.
P Funk amesema hayo wakati wakati kamati Maalum iliyoudwa na COSOTA kukusanya maoni na kushughulikia masuala ya hakimiliki za wasanii ilipokutana kujadili, ambapo P funk ni miongoni mwa wanakamati na viongozi wa kamati hiyo.
Amesema kuwa “Tunafahamu mikutano mikubwa ikitokea, wasanii wakubwa huwa hawapendi kujitokeza, ninachoomba kwao, tukipokea maoni, uamuzi ukatoka sio kwamba mje mlalmike kwamba hamjashirikishwa. Ni muhimu kutambua hilo, wana nafasi ya kuingia mtandaoni na kuweka maoni yao ama kupitia namba ya WhatsApp ambayo imewekwa ili baadaye tuepuke lawama.
Pia amesema kuwa “Kwenye sekta ya Bongo Fleva ndio utamaduni wetu, wanapenda kulalamika lakini vitendo hatuna, ndivyo tulivyo… tumeshafeli huko nyuma, lakini kwa sasa hivi tumejifunza vya kutosha hatuko tayari kufeli tena, tunarekebisha na tutafanikiwa.
“Wasanii mnapokuwa na umoja mnakuwa na sauti moja na fikra moja, ni vizuri tujifunze kukaa chini ya vyama, kwa sababu hata mkiitwa leo na Mhe. Rais Samia Suluhu mkazungumze naye kutoa changamoto zetu au kujadili mambo muhimu kuhusu sanaa, hamuwezi kwenda wote, watakwenda viongozi wenu ambao ndio sauti yenu kwenda kuwawakilisha.
Mwisho amemalizia kwa kusema kuwa “Tumekusanya mirabaha kwa muda mrefu, saa nyingine ilikuwa ikikusanywa lakini mgao hautoki mara utoke, lakini sasa hivi vitu vinakwenda kwa kasi sana. Vitu vikisemwa vitafanyika, vinafanyika. Kwa miaka ya nyuma watu kuelewa maana ya mirabaha na hakimiliki zao ilikuwa ngumu sana, hata wasanii sasa hivi wanaanza kueleawa.