Mwanamuziki wa Bongo Fleva, Ommy Dimpoz amefunguka na kusema kuwa aliwekewa sumu nusura apoteze uhai wake.
Baada ya tukio hilo lilitokea mwaka 2018, Dimpoz alibaki akipambania uhai wake huku akifanyiwa oparesheni tatu maalum za koo katika juhudi za kuokoa maisha yake.
Juzi wakati akitumbuiza katika Kipindi cha Break Point, Dimpoz alisikika akiimab; “Sumu waliniwekea, bado nusu nikufuate mama…”
Hii inatafsiriwa kwamba kwa sasa angekuwa marehemu, kwani ilibaki kidogo amfuate mama yake ambaye ametangulia mbele za haki.
Dimpoz ambaye ameuanza vyema mwaka huu huku tayari akiwa ameachia ngoma mbili, aliwahi kufichua kuwa tatizo la koo lake lilitokana na sumu.
Dimpoz alisema kuwa, sauti yake ilirudi kabla ya kupelekwa nchini Ujerumani ambako alifanyiwa oparesheni ya tatu na ya mwisho.