Mwanamuziki wa Bongo Fleva, Rayvanny ametangaza kuondoka rasmi katika Lebo yake ya WCB na kwenda kuanza maisha mapya nje ya lebo hiyo ambayo ameitumikia kwa miaka sita sasa tangu aliposainiwa mwaka 2016.
Rayvanny amesema sasa ni wakati wa yeye kuondoka WCB ili kuwaachia wengine huku akimshukuru CEO wa WCB, Diamond Platnumz kwa msaada mkubwa wa kumkuza kimuziki na kumtambulisha Duniani.
Kupitia akaunti zake za mitandao ya kijamii ameandika “Waooh! Ni miaka sita sasa tangu tumeanza kufanya kazi pamoja, my team, my family, WCB Wasafi. Umoja, upendo vimekuwa nguzo kubwa sana, kama team, nimejifunza mengi lakini pia mengi tumefanikisha tukiwa pamoja.
“Nimekuwa msanii wa kwanza mwenye Tuzo ya BET, msanii wa kwanza kupanda majukwaa makubwa duniani kama MTV, Dubai Expo na mengine mengi. Nimekuwa msanii wa kwanza kuingia kwenye charts za Billboard, nimekuwa msanii wa kwanza kutoka Afrika Mashariki kupata streams milioni 100 kwenye Boomplay. Haya yote yalifanyika tukiwa pamoja.
“Shukrani za dhati kwa Wasafi, shukrani za dhati kwa my brother Diamond Platnumz kwa kunipa nafasi ili Dunia ione kipaji changu. Namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunifikisha hapa nilipofika, kuisaidia familia yangu na mafanikio mengi katika maisha yangu.
“My brother Diamond Platnumz, heshima yangu kwako haitokaa ifutike, ninathamini sana mchango wako kwangu, Mungu akusaidie, na yote uliyonifanyia, Mungu akuzidishie, Gog Bless You Lion.
“Ila mtoto anayekuwa, anatoka nyumbani anakwenda kuanza maisha na kuipa heshima familia yake. Umenilea, umenikuza, sasa ni muda wangu kuondoka nyumbani na kuanza maisha mengine.
“Lengo ni ukuaji na kuwapa nafasi vijana wengiune. Maana ninapotoka mimi, wengine pia wanaweza kupata nafasi ya kusaidiwa, lakini pia nakokwenda naweza kuwashika mkono vijana wengine kwa sababu hata mimi nilisaidiwa kufika hapa, yangu ni hayo machache. Naitwa Rayvanny ‘Vee vanny Boy’ ‘Chui’ ‘Next Level President,” amemaliza Rayvanny.