Tamasha kubwa la muziki wa dansi nchini linatarajiwa kutimua vumbi jijini Dar keshokutwa Jumamosi likishirikisha bendi tano za muziki wa dansi.
Tamasha hilo lililoandaliwa na Kampuni ya Cheza Kidansi Entertaiment na kudhaminiwa na Kampuni ya Pembejeo za kilimo na Viuatilifu ya Mo Green International Limited chini ya Mkurugenzi wake, Patrick Kessy linatarajiwa kufanyika kwenye viwanja vya Gwambina Lounge zamani TCC Club Dar.
Akizungumza kwenye mkutano na wanahabari Mkurugenzi Mtendaji wa Cheza Kidansi Entertainment, Benard James amesema katika tamasha hilo bendi tano zinatarajiwa kutoana kijasho.
Benard alizitaja bendi hizo kuwa ni Bogoss Muzika chini ya Nyoshi El Saadat, Waluguru Orijino chini ya Killer Boy, Msondo Music Band na Mjengoni Classic chini ya Dijitali na Mapacha Music chini ya Jose Mara.
Katika mkutano huo na wanahabari pia alikuwepo mkongwe wa dansi hapa nchini Komandoo Hamza Kalala a.k.a Mzee Mtukutu ambaye aliyesema naye atakuwepo kwaajili kunogesha tamasha hilo.
Naye Meneja wa Gwambina Lounge Sasiro Ahmad amesema kwa upande wao wameandaa vizuri eneo la tamasha hilo ikiwemo masuala ya usalama na maengineyo.
Sasiro amesema kabla ya burudani hiyo wameandaa luninga za kutosha kwa ajili ya kuangalia laivu mechi ya Watani wa jadi Simba na Yanga inayotarajiwa kufanyika jijini Mwanza.
Wakiwa kwenye mkutano huo na wanahabari wanamuziki wa bendi zinazotarajiwa kushiriki tamasha hilo kila mmoja alimwaga tambi za kuifunika bendi ya mwenzake jambo linaloonekana kuweza kuwa na ukinzani wa aina yake.