Mwanamuziki mkongwe wa Bongo Fleva, Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ amesema safari yake ya muziki haikuwa nyepesi, ingawa hakukata tamaa na kuishi kwenye ndoto zake.

Sugu amesema alilazimika kufanya kazi ya ulinzi ili apate pesa ya kurekodi muziki, hakukata tamaa na ndoto zake zimefanikiwa.

Mwanamuziki huyo ambaye Mei 31 atafanya tamasha la kuadhimisha miaka 30 ya maisha yake ya muziki kwenye hoteli ya Serena, amesema katika tamasha hilo litakaloongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan, mashabiki wake watapata kujua historia ya maisha yake ya muziki, siasa na sasa mfanyabiashara.

“Nakumbuka hata niliposema nakwenda kugombea ubunge, rafiki zangu walicheka na kuniona nimedata (changanyikiwa), lakini sikukata tamaa, hivyo nakwenda kuwahamasisha vijana kutokata tamaa,” amesema.

Amesema tamasha hilo ni la burudani ya muziki na si vinginevyo na baada ya Mei 31 kwenye hoteli ya Serena watakwenda kwenye mikoa mingine mitano nchini.

“Nikiwa kule, nitazungumza na wanafunzi wa vyuo vikuu ambapo Mwanza itakuwa ni chuo cha Sauti, nitakwenda Mbeya, Arusha, Dodoma pale U Dom na Dar es Salaam (UDSM), ambapo nitazungumza na vijanq khhusu kuishi kwenye ndoto zao na kutokata tamaa,” amesema.

Amesema yeye atakuwa ni mfano halisi kwao na baada kongamano kwenye vyuo hivyo, usiku atafanya tamasha kwenye kila mkoa atakapokwenda akishirikiana na wasanii maarufu nchini wa kundi la Weusi, G Nako na Joh Makini, Lady Jay Dee na Ambwene Yesaya.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *