Kundi la muziki nchini Kenya Sauti Sol limetishia kushtaki kampeni za urais za Waziri Mkuu wa zamani Raila Odinga kwa madai ya ukiukaji wa hakimiliki.

Akaunti za mitandao ya kijamii za Odinga zinasemekana kutumia wimbo wa Sauti Sol wa Extravaganza wakati wa kumtambulisha Martha Karua kama mgombea mwenza wa Muungano wa Azimio la Umoja.

Katika taarifa iliyochapishwa kwenye mtandao wa Twitter, Sauti Sol walilalamika kuhusu matumizi ya muziki wao katika kampeni zinazoendelea za kisiasa.

Walisema “hawakuwa na uhusiano wala kuhusishwa na kampeni ya Azimio la Umoja au vuguvugu lolote la kisiasa na/au chama”.

Chama cha ODM, ambacho ni sehemu ya muungano wa Azimio na ambaye Odinga ni mshirika, kilisema wanathamini muziki wa Sauti Sol, na “kucheza wimbo wao ilikuwa kuoesha mapenzi kwa kazi yao”.

Lakini baadhi ya watumiaji wa mtandaoni wameitupia lawama bendi hiyo, wakisema kwamba muungano wa Bw Odinga ulikuwa umelipa Chama cha Hakimiliki ya Muziki Kenya (MCSK) zaidi ya $4,800 ya ada ya leseni ili kutumia kazi za muziki zilizo na hakimiliki katika kampeni yao.

Hata hivyo wasanii wengi wakiwemo Sauti Sol, wamekikosoa chombo cha hakimiliki juu ya muundo wanaotumia kuwafidia. Sauti Sol ni moja ya bendi kubwa barani Afrika na ilishinda Tuzo za Muziki za MTV Africa 2016.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *