Mwanamuziki wa Bongo Fleva, Nandy amezaliwa Novemba 9, 1992 mjini Moshi, Kilimanjaro nchini Tanzania.
Nandy alianza kuimba akiwa na umri wa miaka 6 na alipofikisha umri wa miaka 15, alijiunga na kwaya ya shule, hatua ambayo ilimsaidia kuboresha umahiri wake wa kuimba. Baadaye, aliyekuwa mwandani wake, Ruge Mutahaba; Mtendaji Mkuu wa Tanzania House of Talent (THT) alimchukua na kuikuza sanaa yake.
Wakati wake huko THT, alikutana na producer Emma The Boy ambaye alifanya kazi naye kwenye wimbo wake wa kwanza wa Nagusagusa mwaka 2016.
Awali mwaka 2015, Nandy alikwenda kushiriki Shindano la Tecno Own The Stage nchini Nigeria na kuibuka mshindi wa nafasi ya pili.
Mwaka 2017, aliachia ngoma yake ya One Day ambayo ilitamba na kumpa fursa ya kuwa miongoni mwa wasanii walioshiriki kwenye jukwaa la Coke Studio Africa.
Baada ya hapo, Nandy alianza kutoa ngoma moja baada ya nyingine na sasa ni mmoja wa wanamuziki bora wa kike Afrika Mashariki na Kati.
Baadhi ya nyimbo zake bora ni pamoja na Leo Leo, Number One, One Day, Kivuruge, Aibu, Nibakishie, Hazipo, Acha Lizame, Ninogeshe, Kiza Kinene, Subalkheri, Nigande, Bado, Nimekuzoea, Siwezi na nyingine kibao.
Mwaka wa 2020, Nandy alitangaza rasmi kuwa kwenye uchumba na rapa Billnass au Nenga ambapo ndoa ni Juni, mwaka huu.