Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania(TCRA), imepiga marufuku vyombo vya habari na mitandao ya kijamii kutoonyesha wimbo wa ‘Mtasubiri’ ulioimbwa na msanii Diamond Platnumz akimshirikisha Zuchu.
Video hiyo iliyotoka mwezi mmoja uliopita mpaka sasa imeshatazamwa zaidi ya mara milioni kumi kwenye mtandao wa Youtube na ni moja kati ya nyimbo zilizoko katika EP yake First of All (FOA) ukiwa wimbo namba nne.
Kuzuiwa kwa video hiyo kumetangazwa kupitia taarifa ya TCRA na kuthibitishwa na Meneja wake wa huduma za utangazaji, Mhandisi Andrew Kisaka,alipozungumza na Mwananchi Digital ambaye hata hivyo alitaka kwa maelezo zaidi watafutwe Baraza la Sanaa la Taifa (Basata).
“Ni kweli hiyo ni taarifa yetu, lakini kwa maelezo zaidi watafute Basata kwani wao kiutaratibu ndio wanaleta maombi na sisi tunachofanya ni utekelezaji kama wasimamizi wa vyombo vya utangazaji,” amesema Mhandisi Kisaka.
Katika tangazo hilo linaloonyesha limetolewa Aprili 29, 2022 ikiwa na kichwa cha habari ’Vyombo vya utangazaji kutopiga wimbo wa msanii Nasib Abdul (Diamond Platnumz) kwa kushirikiana na Zuhura Othuman Soud (Zuchu), uitwao ‘Mtasubiri Sana’.
Taarifa hiyo ilieleza kuwa TCRA imepokea taarifa kutoka Basata ya kuzuia usambazaji wa video ya wimbo wa wasanii hao unaopigwa katika mitandao ya kijamii na vyombo vya utangazaji.
Imesema sababu za kuzuia video hiyo ni kutokana na kuwa na kipande kinaonyesha wahusika wapo kanisani wanaimba kwaya lakini baadae wakaacha na kuelekea kwingine.
“Kipande hicho cha video kimeleta ukakasi miongoni mwa waumini wa madhehebu ya dini na kuleta hisia kwamba ni dharau juu ya dini/madhehebu fulani.
“Hivyo kwa baru hii, TCRA inaagiza vyombo vyote vya utangazaji na mitandao ya kijamii hapa nchini kutorusha video ya wimbo uitwao huo ’Mtasubiri’ hadi hapo msanii tajwa atakaporekebisha sehemu hiyo ya video,” ilisomeka sehemu ya taarifa hiyo.