Mwanamuziki wa Bongo Fleva, Nay wa Mitego amesema muziki wake umekuwa ukilenga maisha ya vijana wengi wa mitaani kutokana na ujumbe anaoutumia ndio maana amegeuka kuwa Rais wa Kitaa.
Nay amesema kuwa amekulia kitaani na amekutana na changamoto nyingi ndio sababu ameamua kurudisha kile alichonacho kwa kuwatetea.
“Ukisikiliza mashairi ya kazi zangu nyingi ni ya kutetea wanyonge na nimekuwa nikiwapigania kwa kuwafikishia ujumbe wakubwa tusioweza kuwafikia kirahisi,” alisema mkali huyo wa Nakula Ujana na kuongeza;
“Kuitwa Rais wa Kitaa sijajibatiza mwenyewe, hilo jina ni mapokeo ya kazi zangu kutoka kwa Watanzania na mashabiki wangu wa hali ya chini ambao wanaanini kupitia kazi zangu kufikisha ujumbe.”
Nay amesema anafurahi kuungwa mkono Watanzania wanaofuatilia kazi zake na kumuweka kwenye ushindani kutokana na sapoti zao kila anapotoa kazi mpya.
“Muziki wa HipHop sasa umeingia kwenye ushindani YouTube, nikiachia kazi zinatazamwa sana na kuingia kwenye ushindani tofauti na miaka ya nyuma kulikuwa hakuna mwana hiphop ambaye anaweza kuonyesha ushindani huo na wasanii wa Bongo fleva.”