Mwanamuziki wa Bongo Fleva, Alikiba amerudisha heshima yake aliyoiachia mwaka 2015.

Hivyo ndivyo unavyoweza kusema baada ya kushinda tuzo tano katika utoaji wa tuzo za muziki Tanzania (TMA), rekodi ambayo aliiweka mwaka 2015.

Tuzo hizo zilitolewa jana Jumamosi Aprili 2, 2022 jijini humo, zikiwa ni tuzo za kwanza kusimamiwa na serikali na za kwanza kufanyika tangu zilipoacha kutolewa mwaka 2015.

Katika usiku huo wasanii mbalimbali walipata tuzo, lakini aliyeongoza kupata nyingi ni msanii Alikiba kwa upande wasanii wa muziki wa BongoFleva kwa kupata tuzo tano.

Tuzo alizozoa ni katika kipengele cha Albamu Bora ya Mwaka, mtunzi bora wa melody, mtunzi bora wa mashairi, msanii bora wa kiume Afrika Mashariki na msanii bora wa kiume chaguo la watu.

Hatua hiyo inamfanya Alikiba kurudia historia yake aliyoiweka mwaka 2015 katika tuzo za Kilimanjaro ambapo pia alitunukiwa tuzo tano.

Katika tuzo hizo, msanii huyo anayetesa na wimbo wa ‘Utu’ kwa sasa, alishinda kipengele cha mtunzi bora na mburudishaji bora vipengele ambavyo amevishinda tena mwaka huu.

Kipengele vingine alivyoshinda ni mwimbaji bora wa Bongofleva, wimbo bora wa Afro Pop, kupitiwa wimbo wake wa Mwana ambao pia alishinda nao katika kipengele cha wimbo bora wa mwaka.

Baadhi ya watu waliohudhuria hafla hiyo ya ugawaji tuzo akiwemo Emima Lazaro na Francis Abel, walisema Alikiba amesatahili tuzo hizo na ndio maana hata hakukuwa na zomea zomea hata alipokuwa akitajwa kushinda.

Kwa upande wao uongozi wa Alikiba uliomwakilisha usiku huo kutokana na kuwa safarini, walisema msanii huyo kawashukuru watanzania na kueleza huyo ni zawadi yao kutokana na namna wanavyomsapoti kwenye muziki wake.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *