Mwanamuziki wa Hip Hop Bongo, Wakazi ameibuka na jipya kuhusu kujitoa kwenye tuzo za muziki kwa msanii Nay wa mitego ambaye hivi karibuni alitangaza kujiengua kutokana na kile alichodai kuwa hajaridhishwa na mwenendo mzima wa maandalizi na uendeshwaji wa tuzo hizo.
Wakazi amedhihirisha kuheshimu maamuzi ya Nay, huku akikosoa kitendo cha kujitoa kwenye tuzo hizo hali ya kuwa suala la uwepo wa tuzo kwenye kiwanda cha muziki Tanzania kilikuwa kilio cha muda mrefu na uamuzi wa serikali kuzirejesha ni wa busara licha ya uwepo wa udhaifu kwenye maeneo kadhaa.
Rapa huyo amegusia kuwa wasanii kuendelea kuwepo ndani ya tuzo na kuziunga mkono badala ya kujiengua kutachangia urahisi wa kufanyiwa kazi kwa changamoto hizo ili kuleta mabadiliko chanya kwa manufaa ya tasnia ya muziki nchini.
Aidha rapa huyo ametaja manufaa zaidi ya wasanii wote kwa pamoja kushikamana katika kuziunga mkono tuzo hizo zitolewazo na Serikali kupitia Wizara ya Sanaa, Utamaduni na Michezo chini ya Baraza la Sanaa la Taifa (Basata) na kutoa rai kwa wasanii wengine waliozipuuzia tuzo hizo.
Wakazi ameyasema hayo kupitia maelezo aliyoyavhapisha kwenye ukurasa wake wa mtandao wa Instagram mapema Machi 30, 2022.