Mwanamuziki wa Bongo Fleva, Diamond Platnumz amekosolewa vikali mtandaoni baada ya bendera iliyokuwa inapinga kusitishwa kwa biashara ya utumwa nchini Marekani kuonekana katika video yake mpya iitwayo ‘Gidi’.

Bendera hiyo ilikuwa inawakilisha kundi la majimbo ya kusini ambayo yalipigana kudumisha utumwa wakati wa Vita vya wenyewe kwa wenyewe vya Marekani na bendera hizo zinaonekana kama ishara ya mivutano ya ubaguzi wa rangi nchini Marekani.

Moja ya matukio ya picha hizo za Diamond ina bendera mbili zilizoonyeshwa wakati akicheza huku akiwa na muonekano wa Cowboy.

Baadhi ya watumiaji wa Twitter wametoa hisia zao kuhusiana na video ya msanii huyo baada ya kutoka rasmi wiki hii.

Kufikia sasa Diamond hajatoa tamko lolote kuhusiana na madai hayo. Diamond ambaye ndiye msanii maarufu zaidi katika eneo la Afrika mashariki hajaepuka migogoro katika siku za hivi karibuni.

Mwaka uliopita msanii huyo maarufu alijipata mashakani miongoni mwa wapenzi wa tuzo za BET.

Zaidi ya watu 20,000 walitia saini pingamizi mtandaoni wakitaka wasimamizi wa tuzo hizo kumpiga marufuku mwanamuziki huyo baada ya kuteuliwa kuwania orodha ya mwanamuziki bora wa kimataifa.

Msanii huyo alikuwa akituhumiwa na shirika lisilokuwa la kiserikali Change Tanzania kwa kuunga mkono kile kilichodaiwa kuwa uongozi wa kiimla wa aliyekuwa rais wa taifa hilo John Pombe Magufuli.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *