Miaka mitano ya mapenzi na uchumba uliogubikwa na milima na mabonde tangu mwaka 2016, lakini hatimaye wazazi wa Malkia wa Bongo Fleva, Faustina Charles almaarufu Nandy wamemkubali mchumba’ke, William Lyimo au Billnass na sasa ndoa inanukia.
Katika kipindi chote hicho cha mapenzi yao, Nandy au Nandera na Billnass au Nenga waliripotiwa mara wameachana na mara wamerudiana.
Miongoni mwa sababu hizo, yapo madai kwamba, upande wa Nandy; yaani ukweni au wazazi na baadhi ya ndugu hawakuwa wakimkubali Nenga awe mkwe au shemeji yao, lakini sasa wamekubali muziki na posa ya jamaa huyo.
Hata hivyo, kuhusu suala la kukataliwa ukweni, Nenga aliwahi kulikanusha akisema; “Sidhani kama ni kweli, lakini pia wakwe zangu mimi ni watu wa dini sana, hivyo nisingependa kuwaongelea sana kwenye media yoyote ile kwa sababu ninachokijua mimi ni kwamba, wananipenda kama mtoto wao na wamenikubali.”
Habari za ndani zinaeleza kwamba, kwa sasa kopa la wawili hao limejaa upya baada ya kwenda kujiachia Dubai kisha kurejea kwa wazazi wa Nandy ambapo Nenga alionekana akiwa amepiga picha na baba na mama wa mpenzi wake huyo, jambo ambalo awali halikuwahi kutokea.
Kabla ya kusambaa kwa picha ya Nenga na wazazi wa Nandy, jamaa huyo aliposti picha kwenye ukurasa wake ikimuonesha mrembo huyo na mama wa jamaa huyo na kuandika; “My Mommy and her best friend! Mtu na mkwe wake! Naipenda sana hii picha na nawapenda sana walioko kwenye hii picha Inshaalah kuna siku nitawaongezea rafiki yao mwingine nitakayempenda Zaidi.