Mwanamuziki wa Bongo Fleva, AT amedai kuwa, msanii wa Bongo Fleva, Harmonize ni sawa na Fidel Castro wa Bongo kwenye muziki huo maana kila vita vya kisanaa inayokuja mbele yake amekuwa akiishinda bila taabu.
Utakumbuka Fidel Castro aliongoza mapinduzi nchini Cuba yaliyomtoa madarakani Rais Dikteta Fulgencio Batista mwaka 1959; alikuja kuwa Waziri Mkuu wa kwanza wa nchi hiyo na baadaye Rais hadi mwaka 2006.
Katika utawala wake, Castro hakukubaliana na Marekani na kuamua kujiunga na siasa za Ukomunisti zilizokuja kuporomoka duniani kote mwaka 1989.
Hata hivyo, tayari alikuwa ni adui wa Marekani, maofisa wa ujasusi wa nchi hiyo (CIA) walijaribu kumuua katika kisa kilichojulikana kama Operation Mongoose ambapo walipanga kumpa Castro sigara yenye vilipuzi, lakini mbinu hiyo na nyingine nyingi hazikuweza kufua dafu.
AT aliyetamba na Kundi la Offside Trick kutoka Visiwani Zanzibar anasema kuwa, ameamua kumpa Harmonize jina hilo kwa kuwa Castro alisaidia baadhi ya nchi za Afrika kupata uhuru, jambo ambalo ni sawa na hatua ya Konde Boy kumrejesha yeye kwenye muziki baada ya kufanya kazi nyingi bila mafanikio.
“Halafu unajua Fidel Castro ambaye amepigana vita vingi bila kupigwa alikuwa na ukaribu mkubwa sana na Tanzania, kwa hiyo Harmonize tumempa cheo hicho kwa sababu ni Mwanajeshi na yeye mwenyewe anajita Jeshi, anapigwa vita kimuziki, lakini bado anasonga,” anasema AT.