Serikali imesitisha utekelezaji wa kanuni za kukagua nyimbo za wasanii kabla hazijapelekwa kwenye redio, televisheni na majukwaa mbalimbali.
Uamuzi huo umetolewa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Innocent Bashungwa alipokutana na wadau wa muziki nchini wakiwemo wasanii mkoani Dar es Salaam.
Kanuni hizo ni za sheria namba 23 ya mwaka 1984 ya Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) pamoja na marekebisho yake ya mwaka 2019.
Kanuni hizo namba 25 kifungu (1)-(8) inaeleza kuhusu masharti mahususi juu ya masuala ya maadili ya kazi za sanaa na utoaji wa ithibati katika kazi za sanaa.
Bashungwa amechukua uamuzi huo baada ya wadau wa muziki kupinga suala hilo wakidai haliwatendei haki ikiwa ni baada ya BASATA kuzuia wimbo wa Mama wa msanii Ney wa Mitego kwa maelezo kuwa una mashairi yenye ukakasi.