Rais wa Zimbabwe, Robert Mugabe ameifuta ziara ya nchini Ghana kupokea tuzo ya Millennium Lifetime Achievement award kwa kuliongoza taifa hilo la kusini mwa Afrika kupata uhuru wake mwaka 1980.
Rais wa Ghana, John Mahama alitarajiwa kumpa Mugabe tuzo hiyo wakati wa warsha ambayo ingefanyika katika mji mkuu wa Ghana, Accra.
Mugabe mwenye umri wa miaka 92 ameingoza Zimabawe tangu ipate uhuru na ameapa kusalia madarakani hadi kifo na kukataa wito wa kumtaka ang’atuke.
Hakuna sababu iliyotolewa ya kufutwa kwa safari hiyo lakini mtandao mmoja nchini Ghana unawanukuu wanadiplomasia nchini Zimbabwe wakisema kuwa hatua hiyo ilichukuliwa kutokana masuala ya kisiasa nchini Zimbabwe.
Mabango makubwa yalikuwa yamewekwa mjini Accra kumkaribisha Rais Mugabe na pia hotuba yake ilikuwa imesubiriwa kwa hamu kubwa na wananchi wa Ghana.