Mwanamuziki wa Bongo Fleva, Linex amesema hana mambo mengi zaidi ya kufanya kazi iliyo na ujumbe kwa jamii inayosikiliza nyimbo zake, jambo linalomfanya asiwe na haraka ya kuachia nyimbo mara kwa mara.

Linex amesema kuwa mashairi yake yanazingatia changamoto zilizopo kwenye jamii, hivyo anakuwa anaangalia namna ya kutoa faraja ama funzo, kupitia uimbaji wake unaokuwa umejaa hisia kali hata wakati wa uwasilishaji wake.

“Ninachokiimba kinatokana na jamii inayonizunguka ama jamii ya Watanzania, ndio maana nyimbo zangu sio za kusikiliza mara moja ama mbili zikafa, hadi leo zikipigwa zina maana kubwa ambayo inakuwa inafunza ama kufariji,” amesema na ameongeza kuwa;

“Licha ya kwamba sokoni kuna ushindani mkali, binafsi haunisumbui kutokana na mashairi yangu kuwafikia walengwa ama masikio yao kuwa na tafsiri kuliko kuburudika na mdundo kisha wakasahau, ninacholenga ujumbe kuishi mioyoni mwao,”amesema.

Linex ambaye amewahi kutamba na nyimbo mbalimbali ikiwemo Halima, Kesho yangu, Wema kwa Ubaya, Nitaificha Wapi na nyinginezo amesema wakati wowote kuanzia sasa ataachia albamu yake yenye nyimbo za dini na za bongo fleva.

“Baada ya kimya kirefu nakuja kwa kishindo, kikubwa mashabiki wangu wakae mkao wa kusikiliza nyimbo kali sana, naamini zitawajenga, zitawafariji na wataijua jamii kwa mapana yake,”amesema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *