Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imekiruhusu kituo cha televisheni, Wasafi TV, kuanza tena kurusha matangazo kuanzia Machi Mosi 2021, baada ya kupunguza adhabu waliyopewa.
Januari 5, 2021 TCRA ilitoa uamuzi wa kuifungia Wasafi TV kwa kipindi cha miezi sita kutokana na kukiuka Kanuni za Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta, kwa kurusha maudhui ambayo yameonyesha maungo ya mwili wa mtu.
Januari 21 Wasafi TV iliwasilisha TCRA maombi na vielelezo zaidi ikiiomba mamlaka hiyo kupitia upya uamuzi wake.
Januari 28 wakati wa kusikilizwa kwa maombi yao, kituo hicho kiliwasilisha ushahidi mpya, na kueleza kuwa endapo ungezingatiwa awali, kisingepewa adhabu ya kufungiwa kwa miezi sita. Kituo hicho kilikiri kurusha matangazo mubashara kinyume na masharti ya leseni yao na kuomba kupunguziwa adhabu waliyopewa.
Taarifa iliyotolewa leo Februari 4, 2021, na Mkurugenzi Mkuu wa TCRA imeeleza kuwa Wasafi TV itaendelea kutumikia adhabu hiyo mpaka Februari 28, 2021.
Aidha, imeelekezwa kuzingatia masharti ya leseni ya kutoa huduma za maudhui ya kulipia kwa njia ya televisheni na iwapo itashindwa, itakataa, au kukaidi uamuzi huo, hatua zaidi za kisheria na kiudhibiti zitachukuliwa dhidi yao.