Mwanamuziki wa Hip Hop nchini, Hamis Mwinjuma ‘Mwana FA’, amesema baada ya kupata nafasi ya ubunge wa Jimbo la Muheza juhudi zake anazihamishia kwa wananchi wa huko.
Mwana FA alitangazwa kushinda kiti cha ubunge kwa tiketi cha Chama cha Mapinduzi (CCM) kwa jimbo hilo kwa kura 47,578 akifuatiwa na Yosepher Komba (Chadema) mwenye kura 12,034.
Mwana FA alisema kwa sasa muziki utasubiri kwanza kidogo ili afanye kazi ya wananchi kwa kujipanga kuwasemea wapiga kura wake na kutatua matatizo yao.
“Kitu ninachoangalia kwa sasa ni namna gani nitawatumikia wananchi wangu walioniamini na kunichagua. Nina deni kubwa kwao kuhakikisha nayabeba matatizo yao, kama muziki ni kitu ambacho hakichukui muda mrefu kurekodi naweza kufanya baadaye,” alisema.
Aliwashukuru wananchi wa huko kwa imani kubwa waliyomuonyesha na kwamba anamuomba Mungu amsaidie aweze kutimiza kile alichokusudia.
Kuhusu wasanii wenzake wa vyama vya upinzani waliongushwa katika uchaguzi Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ na Joseph Haule ‘Professa Jay’ alisema anasikitishwa ila anawahimiza kuhamia kwenye chama chenye misimamo yake (CCM) kama itawapendeza.
“Natamani na wao wangekuwa ni wana Chama Cha Mapinduzi tuwe pamoja. Ningependa wawe kwenye chama nilichopo, ni chama chenye msimamo wake,” alisema.