Jumuiya ya Dawoodi Bohra imetoa shilingi milioni 116 kwa ajili ya kuunga mkono kampeni ya kuchangia madawati inayoendelea hapa nchini.
Hatua hiyo imetangazwa na Kiongozi Mkuu wa Jumuiya hiyo Mtukufu Dkt. Syedna Mufaddal Saifuddin Saheb(TUS) leo Ikulu Jijini Dar es Salaam, alipokuwa akifanya mazungumzo na Rais wa Tanzania, Dkt John Pombe Magufuli.
Mtukufu Dkt. Syedna Mufaddal Saifuddin Saheb amemkabidhi Rais Magufuli hundi ya Dola la Marekani Elfu Hamsini na Tatu (USD-53,000) sawa na Shilingi Milioni 116 za Kitanzania kwa ajili ya kuchangia utengenezaji wa madawati ya wanafunzi kwa shule mbalimbali hapa nchini.
Pia amekabidhi hundi ya Dola za Marekani Elfu Ishirini na Moja (USD-21,000) sawa na Shilingi Milioni 46 kwa ajili ya Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA).
Katika hatua nyingine, Rais Magufuli amepokea barua kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Kiarabu ya Saharawi Mhe. Brahim Ghali iliyowasilishwa na Mjumbe Maalum wa Rais huyo ambaye ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Mhe. Bachir Moustapha Sayed.
Pamoja na kupokea barua hiyo Rais Magufuli amesema Serikali yake ya Awamu ya Tano itaendeleza na kuimarisha zaidi ushirikiano wake na Jamhuri ya Kiarabu ya Saharawi na pia itaendelea kuunga mkono juhudi za wananchi wa Saharawi kupata haki ya kuamua hatma yao.