Mwanamuziki wa Bongo Fleva, Harmonize amesema kuwa ameuza nyumba zake tatu pamoja na mali nyingine kuilipa WCB kiasi cha Tsh milioni 500 ili kuvunja mkataba.
Harmonize amesema kuwa aliamua kuuza vitu hivyo ili ailipe lebo yake hiyo ya zamani kutokana na vipengele vilivyowekwa kwenye mkataba wake wa kazi wakati anasaini kwenye lebo hiyo miaka ya nyuma.
Pia mwanamuziki huyo amesema kuwa ni kweli kwasasa hayupo sawa na uongozi wake wa zamani uliopita baada ya kutangaza kuondoka kwenye lebo hiyo iliyomkuza ya WCB chini ya uongozI wa Diamond Platnumz.
“Ukweli hatupo sawa na uongozi uliopita, sitaki kusema uongo, mahusiano yangu na uongozi uliopita sio kama zamani. Naomba niwashukuru kwa sababu wao ndo wamesababisha mimi kuwa hapa” Alisema Harmonize
“Mkataba wangu ulikuwa unanitaka nilipe shilingi milioni 500 kama nikiondoka ili niweze kupata hakimiliki ya jina langu pamoja na nyimbo zangu. Hivyo sikuwa na hela kabisa. Nimeuza nyumba zangu tatu na baadhi ya mali, deni limebaki kidogo. Aliongeza Harmonize.
Pia mwanamuziki huyo amesema kuwa licha ya hayo yote lakini hana tatizo lolote na uongozi wa WCB licha ya kuondoka kwenye lebo yake hiyo ya zamani.
Kwa upande mwingine Harmonize ameweka wazi kuwa kwenye albamu yake mpya amefanya nyimbo pamoja na wasanii kama vile Jidenna, Cassanova na Morgan Heritage ambao wote watasikika kwenye albamu yake mpya.
“Kwenye album yangu nimefanya na Jidenna, Cassanova na Morgan Heritage. Nilitamani kuachia album yangu mwisho wa mwaka huu, itakuwa ni ya kuunganisha muziki na wasanii wa Afrika Mashariki pamoja na Magharibi” Alisema msanii huyo
Harmonize kwasasa ameachia wimbo wake mpya unaokwenda kwa jina la Uno ambao ameuachia leo Oktoba 24 ambao unaonekana kupokelewa vizuri na mashabiki wake kutokana na uzuri wa wimbo huo.