Mwanamuziki mkongwe wa rhumba nchini Congo, Koffi Olomide amehukumiwa miaka miwili jela baada ya kupatikana na hatia ya kumbaka mmoja wa wanengeuaji miaka 15 iliyopita.

Amehukumiwa miaka miwili gerezani na mahakama ya Ufaransa akiwa hayupo, baada ya kukosa kufika mahakamani.

Uamuzi huo una maana kwamba nyota huyo wa Congo atakamatwa iwapo atafanya uhalifu mwingine sehemu yoyote.

Olomidé, mwenye umri wa miaka 62, aliagizwa alipe Euro 5,000 kwa madhara aliyomsababishia mnenguaji wake huyo wa zamani.

Mahakama ya Nanterre, nje ya mji mkuu Paris, pia ilimuagiza alipe faini ya kiwango sawa na hicho kwa kuwasaidia wanawake watatu wengine kuingia nchini Ufaransa kwa njia haramu.

Wakili wa Olomidé amepongeza uamuzi huo na kuutaja kuwa ushindi, akiwataarifu waandishi wa habari kwamba uamuzi huo utachangia kuondolewa hati ya kimataifa ya kumkamata popote alipo.

Wanenguaji wanne waliokuwa wakimfanyia kazi wameiambia mahakama kwamba aliwanyanyasa kingono mara kadhaa kati ya mwaka 2002 na mwaka 2006 nchini. Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo na Ufaransa.

Wanawake hao pia walieleza kwamba walizuiwa kwa lazima katika nyumba moja nje ya mji wa Paris na walifanikiwa kutoroka usiku wa Juni 2006, lakini hawakurudi DR Congo kutokana na kuogopa kutafutwa na kulipizwa kisasi.

Waendesha mashtaka walikuwa wakishinikiza ahukumiwe miaka saba gerezani lakini mahakama imetupilia mbali mashtaka ya unyanyasaji na madai ya utekaji nyara.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *