Familia ya Ruge Mutahaba ambaye amefariki dunia hapo jana nchini Afrika Kusini, imeweka wazi kilichotokea mpaka Ruge akakutwa na mauti, akiwa hospitali akiendelea na matibabu ya figo ambayo ilikuwa ikimsumbua.
Mombeki Barego ambaye ni ndugu wa Ruge Mutahaba amesema kwamba jana asubuhi Ruge aliamka huku presha yake ikiwa haiko sawa, lakini licha ya madaktari kufanya jitihada zao ili kumuweka sawa, ilishindikana na kusababisha kupoteza maisha.
Mombeki ameendelea kwa kusema kwamba utaratibu wa kurudisha mwili wa marehemu unaanza kufanyika, huku akiwashukuru watu waliojitokeza kuifariji familia yao.
Ruge Mutahaba alikuwa mmoja wa waasisi wa Clouds Media Group na mmoja ya watu aliochangia kukuza sanaa ya bongo kwa kuibua wasanii mbali mbali, na atakumbukwa kwa mchango wake mkubwa kwenye maisha ya vijana wengi.
Ruge alianza kusumbuliwa na tatizo la figo mwishoni mwaka 2018 ambapo alilazwa katika hospitali ya Kairuki, na baadaye kuhamishiwa nchini Afrika Kusini ili kupata matibabu zaidi, mpaka kifo kilipomkuta Februari 26, 2019.