Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi CUF, Maalim Seif Sharif Hamad ameitaka serikali iliyopo madarakani visiwani Zanzibar inayoongozwa na Dkt. Ali Mohamed Shein iwahurumie wananchi hasa katika kipindi cha mfungo wa mwezi wa Ramadhani.
Akizungumza na waandishi wa habari katika Ofisi za CUF Vuga mjini Zanzibar, amesema kuwa waliopo madarakani wasiwe hodari kuwataka wafanyabiashara wasipandishe bei za bidhaa wanazouza lakini na wao kodi ambazo hazina tija, zinawakamuwa wananchi waweze kuzipunguza.
“Ni vyema kujifunza kwa serikali ya Kenya ambayo imeweza kuondoa kodi kwa wafanyabiashara wale wote ambao watafanya biashara ya tende katika Mwezi wa Ramadhani”, amesema Maalim Seif.
Aidha, Maalim Seif amewataka wananchi kufanya mambo ya kheri katika mwezi huo na kuacha kulumbana, kutoleana maneno yasiyofaa kwani mwezi huo ni mwezi wa rehema hivyo ni vyema kufanya mambo ya kheri yanayompendeza Mungu.
“Ni vyema kupendana,kusaidiana, kuhurumiana,kuacha kugombana na kutohasimiana ili kupata fadhila za Mwezi Mungu”, amesisitiza Maalim Seif.
Kwa upande mwingine, Maalim Seif amewataka wafanyabiashara wasiuchukulie kwamba mwezi wa Ramadhani kama ni msimu wa kupata faida ya kupindukia na badala yake wauchukulie ni mwezi wa kuchuma thawabu kwa lengo la kuwasaidia wananchi hasa masikini.