Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Inspekta Jenerali (IGP) Simon Sirro, amewataka makamishna wastaafu wa jeshi hilo, kuendelea kukabiliana na uhalifu wawapo uraiani kwa kuwa mapambano ya uhalifu hayana mipaka.
IGP Sirro alisema hayo juzi wakati wa hafla maalum ya kuwaaga waliokuwa makamishna wa polisi, Glodwing Mtweve na Elice Mapunda, katika viwanja vya Chuo cha Taaluma ya Polisi Dar es Salaam. Hafla hiyo ilihudhuriwa na maofisa wakuu wa polisi, askari na familia za wastaafu hao.
Mtweve aliwataka maofisa na askari polisi kuendelea kufanya kazi kwa kujituma na weledi ili kuhakikisha uhalifu unaendelea kupungua kwa kuwa sasa unafanywa kisayansi.
Mtweve alisema wanaoendelea kulitumikia Jeshi la Polisi hawana budi kuyafuata yale mazuri yote waliyofanya na yale mabaya kuyaacha ili wamalize salama utumishi wao na kuagwa kama ilivyokuwa kwao.
Naye Kamishna Mapunda, ambaye alikuwa mwanamke wa kwanza kufikia cheo cha kamishna wa Polisi tangu kupata uhuru, aliwataka askari wa kike nchini kujituma ili kupata mafanikio kama ilivyo kwa wanaume kwa kuwa kupata vyeo ndani ya jeshi hilo hakuangalii jinsia bali utendaji wa kazi.
Alisema askari wa kike hana tofauti na wa kiume kwa kuwa mafunzo wanayopitia ni ya aina moja, hivyo wakijituma zaidi na kufanya kazi kwa ufanisi wataonekana na kupewa madaraka kwa mujibu wa taratibu na kanuni za jeshi hilo.