Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hamisi Kigwangalla amesema kuwa mapato yanayotokana na utalii yameongezela kutoka Dola za Marekani Bil. 1.7 mwaka 2012 hadi kufikia Dola za Marekani Bilioni 2.2 mwaka 2017.
Kigwangalla amesema hayo alipokuwa akifungua Warsha ya Kitaifa ya Mapitio ya Rasimu ya Sera ya Taifa ya Utalii ya mwaka 2018.
Aidha amesema, mafanikio ya Sekta ya Utalii yamechangiwa kwa kiasi kikubwa na uwepo wa Sera ya Taifa ya Utalii ya mwaka 1999 na juhudi za Serikali kutekeleza Sera hiyo kwa ushirikiano na wadau katika usimamizi, uhifadhi na matumizi endelevu ya rasilimali za utalii, utangazaji katika masoko mbalimbali ya utalii duniani na mazingira bora ya uwekezaji.
Dkt. Kigwangalla ametaja masuala ambayo yametiliwa mkazo katika Sera hiyo kuwa ni pamoja na Serikali kuendelea kushirikiana na wadau wote wa utalii katika kuhifadhi rasilimali za utalii, kuendeleza rasilimali watu, kuimairisha ushirikiano wa kikanda na kimataifa, kuimarisha mnyororo wa thamani katika mazao ya utalii pamoja na kuongeza wigo wa mazao ya utalii (kama vile kuendeleza utalii wa fukwe na utalii wa mikutano).
Vile vile kuweka mkazo katika kutangaza Tanzania kama kituo bora cha utalii kimataifa, kuweka mazingira wezeshi kwa wawekezaji, pamoja na kuhamasisha utalii wa ndani na kuendelea kusimamia viwango vya ubora wa huduma za malazi nchini.