Serikali imesema hakuna mgonjwa yeyote aliyehisiwa au kuthibitishwa kuwa na virusi vya ugonjwa wa Ebola hapa nchini na kuwataka wananchi kuchukua tahadhari kubwa dhidi ya ugonjwa huo ambao umeripotiwa hivi karibuni katika nchi jirani ya Demokarasia ya Kongo (DRC).

Kauli hiyo imetolewa leo na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma.

Waziri Ummy amesema kuwa hata hivyo taarifa hiyo haiizuii Tanzania kuchukua hatua thabiti dhidi ya kujikinga na ugonjwa wa Ebola kwa kuwa inapakana na nchi ya DRC ambapo kuna mipaka mingi ambayo watu huwa wanaingia na kutoka kwa njia zisizo za halali.

 Aidha, Waziri Ummy amewataka watu wanaoishi katika mikoa inayopakana na nchi ya DRC kuchukua tahadhari pale wanapohisi kupata magonjwa yenye dalili za Ebola kwa kuwahi kufika kwenye hospitali zinazotoa huduma ili wafanyiwe vipimo vya kina kuonyesha kama wameathirika au la.

Waziri Ummy ameitaja mikoa ambayo inapakana na nchi ya DRC kuwa ni Mwanza, Kagera, Kigoma, Katavi, Rukwa na Songwe na kuwataka wananchi wanaoishi katika mikoa hiyo kuchukua tahadhari kubwa ya kujikinga na ugonjwa wa Ebola.

Kwa upande mwingine, Waziri Ummy amesema Wizara imechukua hatua mbalimbali ili kudhibiti ugonjwa huo ikiwemo kutoa taarifa ya tahadhari ya ugonjwa wa Ebola kupitia kwa makatibu tawala na waganga wakuu wote wa mikoa kwa kujumuisha na namna mgonjwa anavyoweza kutambuliwa, namna ya kuchukua sampuli na namna ya kuwahudumia wagonjwa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *