Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa ametoa siku tatu kwa wafanyabiashara na wenye viwanda vya mafuta ya kupikia na sukari nchini kuhakikisha bidhaa hizo zinaendelea kupatikana katika maeneo yote na kwa bei ya kawaida.

Waziri Mkuu ametoa agizo hilo jana Bungeni Jijini Dodoma mara baada ya Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Bw. Charles Mwijage kutoa kauli ya Serikali kuhusu uhaba wa mafuta ya kupikia nchini.


Pamoja na hayo, Waziri Mkuu ameendelea kwa kusema “kama uhaba wa bidhaa hiyo utaendelea, ifikapo Jumapili serikali itaanza kufanya msako kwenye viwanda na maghala na kuchukua hatua kali kwa watakaobainika kuficha mafuta hayo”.

Waziri Mkuu amesema takwimu zinathibitisha kwamba mafuta ya kupikia yaliyoingizwa nchini yanatosha, hivyo nchi haipaswi kuwa na uhaba.

Amesema kuwa “Hatuwezi kukubaliana na jambo hili kwa sababu haliko kwa bahati mbaya ni mpango uliopangwa kwani imekuwa ni kawaida kila tunapoelekea kwenye Mwezi Mtukufu wa Ramadhani kunakuwa na upungufu wa bidhaa hasa sukari, hivyo Serikali haitakubali wananchi wateseke bila sababu za msingi,”.

Akiwasilisha kauli ya serikali Bungeni, Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Bw. Mwijage amesema vyanzo vinavyotumika kuzalishia mafuta nchini vinatosheleza mahitaji kwa asilimia 30, hivyo asilimia 70 ya mafuta huagizwa kutoka nje ya nchi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *