Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli amefunguka na kusema watu ambao wanasema elimu imeshuka nchini wanakosea kwani kuna sehemu ambazo elimu inaonekana ipo vizuri akitolea mfano wa chuo cha kilimo cha Sokoine University of Agriculture (SUA).
Magufuli amesema hayo leo akiwa katika ziara yake mkoani Morogoro na kusema kuwa watu wasiseme kwa ujumla kushuka kwa elimu ili hali kuna sehemu watu wanafanya vizuri katika elimu, na kudai kuwa wa SUA wameweza kufundisha mpaka Panya na akaelewa hivyo ni wazi kuwa wapo vizuri sana.
Rais Magufuli aliendelea kuzungumzia jambo hilo na kusema kuwa walimu wa SUA na wanafunzi wapo vizuri sana katika masuala ya shule ndiyo maana wanaweza kufanya gunduzi mbalimbali ambazo zinatija na msaada katika maisha ya kila siku.
Mbali na hilo Rais Magufuli amekiri kuwa katika awamu yake ya tano wamekuja na elimu bure na kusema kuwa huenda baadae ikaja kuwa na madhara ila itasaidia kuondoa ujinga kwa watu wengi ambao walikuwa wakikosa elimu hiyo kwa sababu ya kukosa ada ya kulipa shule.
Rais mstaafu wa awamu ya tatu Mhe. Benjamini Mkapa miezi kadhaa iliyopita aliwahi kusikika akisema kuwa kuna haja ya kuwa na mjadala wa kitaifa kuhusu elimu ya Tanzania kwa madai kuwa kuna unadhaifu mkubwa na kushukwa kwa kiwango cha elimu ya Tanzania.