Naibu katibu mkuu wa Chadema Zanzibar, Salum Mwalimu (Chadema) amefungua kesi akipinga matokeo ya uchaguzi mdogo uliofanyika Februari 17 katika jimbo la Kinondoni na Maulidi Mtulia kushinda.
Mtulia aliibuka mshindi kwa kura 30,313 dhidi ya 12,353 alizopata Mwalimu. Uchaguzi huo ulifanyika kutokana na Mtulia kujivua ubunge wa jimbo hilo akiwa CUF na kujiunga na CCM iliyompitisha kugombea.
Mwalimu amefungua kesi dhidi ya Mtulia; msimamizi wa uchaguzi ambaye ni mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).
Mbali ya kesi ya msingi namba 129 ya mwaka 2018, Mwalimu amefungua maombi ya kusamehewa au kupunguziwa kiwango cha fedha anachopaswa kukiwasilisha mahakamani kama dhamana kwa ajili ya usikilizwaji wa kesi hiyo.
Katika kesi ya msingi, Mwalimu anaiomba mahakama itengue matokeo na itamke kuwa uchaguzi ulikuwa batili, pamoja na mambo mengine akidai uligubikwa na kasoro nyingi na mwenendo mbaya.
Anadai Naibu Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson wakati wa kampeni alitoa kauli za ubaguzi.