Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt John Pombe Magufuli ameviagiza vyombo vya dola, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kuchunguza mradi wa ujenzi wa jengo la ukumbi wa mihadhara na ofisi za Wahadhiri katika Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Mkwawa (MUCE) kilichopo Manispaa ya Iringa.
Rais Magufuli ambaye alisoma chuoni hapo wakati ikiwa shule ya sekondari ya Mkwawa, ametoa agizo hilo wakati alipotembelea chuo hicho na kuzungumza na wanafunzi na Wahadhiri katika uwanja wa michezo.
Ujenzi wa jengo la ukumbi wa mihadhara na ofisi za Wahadhiri ulianza mwaka 2010 ambapo mpaka sasa serikali tayari imeshatoa shilingi Bilioni 8 na Milioni 804, lakini ujenzi wake bado haujakamilika.
Pamoja na hayo, Dkt. Magufuli ameendelea kwa kusema “huyo Profesa Mushi yuko wapi?, hata kama amestaafu atafutwe aje ajibu hizi hoja, inawezekana amekula hela ya kutosha halafu akastaafu moja kwa moja na kuenda kuanzisha biashara huko”.
Kwa upande mwingine, Rais Dkt. Magufuli ameagiza vyombo vinavyohusika vifuatilie kesi iliyofunguliwa dhidi ya Mkandarasi aliyekuwa akijenga majengo hayo.